Thursday, March 8, 2012

King Messi aweka rikodi ulaya ( UEFA )


Magoli matano kutoka kwa Mchezaji bora wa dunia kwa mara mbili mfululizo raia wa Argentina, Lionel Messi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, hatua ya 16 bora yameweka rekodi mpya kwa mchezaji mmoja kufunga idadi ya mabao hayo katika mechi moja kwenye mashindano ya ngazi ya vilabu yanayoandaliwa na chama cha soka barani Ulaya (UEFA).

Ikicheza nyumbani, Camp Nou, mbele ya mashabiki wake Barcelona iliitandika bila ya huruma Bayer Leverkusen 7 – 1. Ushindi mkubwa waliowahi kupata Barcelona katika uwanja wa nyumbani kwenye mashindano ya ngazi ya UEFA.

Messi alipatia Barcelona magoli kunako dakika za 24, 42, 49, 58 na 84 huku kinda Cristian Tello akitupia nyavuni magoli mawili katika dakika za 62 na 65 katika mechi yake ya kwanza katika mashindano ya UEFA.

Leverkusen walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Karim Bellarabi katika dakika za nyongeza.

Baada ya ushindi wa 3 – 1 katika mechi ya kwanza nyumbani kwa Leverkusen, Barcelona imesonga kwenye hatua ya robo fainali kwa jumla ya mabao 10 – 2.

Katika mechi nyingine APOEL Nicosia iliitandika Lyon 1 – 0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 1 – 1 baada ya wao kufungwa la Lyon 1 – 0 katika mchezo wa kwanza. Hata hivyo Nicosia walisonga katika robo fainali baada ya kushinda kwa mikwaju ya penati.