Monday, March 12, 2012

Mario Balotelli na Yaya Toure nusura wazichape kavukavu

Wachezaji wa Manchester City Mario Balotelli na Yaya Toure nusura wazichape kavukavu wakati timu zinaenda mapumziko kwenye mechi dhidi ya Swansea City kwenye mfululizo wa mechi za ligi kuu ya Uingereza hapo jana, Mechi hiyo iliisha kwa Manchester City kulala kwa bao moja bila majibu.

Chombo cha habari cha The Sun kilieleza kuwa utata huo ulizuka baada ya wachezaji hao wawili kuanza kurushiana maneno kwa sauti kali wakati wakielekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.Iliwachukua muda kidogo wachezaji hao kurejea dimbani kuendelea na mchezo huo wakati kipindi cha pili kilipoanza.

Wakati wanaelekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo Balotelli na Toure walionekana wakitetea jambo fulani kwa umakini wa hali ya juu. Lakini mambo yalibadilika walipoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na wakasikika wakikaripiana kwa hasira. Ingawa kocha wao Roberto Mancini alisema hajui lolote kuhusiana na suala hilo.

Alipoulizwa, kocha huyo raia wa Italia alisema “Hapana, sijui lolote kusiana na suala hilo.”