Thursday, March 8, 2012

Teknolojia kwa shule za msingi Zanzibar


MRADI wa Elimu wa Karne ya 21, unaohusiana na elimu ya teknolojia ya habari na mawasiliano kwa shule za msingi, umetajwa kuwa chachu ya maendeleo katika ulimwengu wa utandawazi.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo jana katika uzinduzi wa mradi huo na kuongeza kuwa watoto wa darasa la kwanza hadi la nne watakuwa wakitumia kompyuta.

Alisema Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ina umuhimu kwa ulimwengu wa sasa na hasa kwa watoto katika kukuza elimu yao ambapo hatua hiyo itawasaidia katika ugunduzi wa maarifa mapya katika masomo, kuchemsha bongo, kurahisisha ufanyaji wa kazi zao na kuokoa muda.

Dk. Shein pia alisisitiza kuwa mabadiliko ya kielimu yanategemea mchango wa walimu wenye kubadilika kitaaluma na katika mbinu za ufundishaji na kueleza kuwa lazima walimu wajifunze kutumia vifaa vya kisasa yakiwemo matumizi ya kompyuta.

Dk. Shein alisema Serikali itaendelea kuwatengenezea mazingira bora walimu ili wazidi kupata moyo katika kutekeleza majukumu yao na kutoa wito kwa walimu kuendelea kuchapa kazi.

Dk. Shein alipongeza uamuzi wa Serikali ya Marekani kwa kupitia Shirika lake la Maendeleo (USAID) kwa kutoa msaada huo unaogharimu dola za marekani milioni 50 ambao utakuwa wa miaka mitano.

Naye Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhardt alisema mradi huo ni msingi muhimu wa kuleta mabadiliko makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano Zanzibar.

Aidha, Balozi Lenhardt alisema kuwa elimu ina umuhimu kwa vijana wa Tanzania kwani ndio silaha katika maisha yao na kusisitiza kuwa mradi huo utakapomalizika unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya walimu 4,094, shule za msingi na sekta za elimu.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zahra Ali Hamad alisema mradi huo utaweza kuwasaidia walimu na wanafunzi kupata taaluma ya teknolojia ya habari na kuzidisha uimarishaji wa sekta ya elimu nchini.

Awali Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mwanaidi Saleh alieleza kuwa mbali ya kushughulikia utoaji wa elimu kwa walimu na wanafunzi, mradi huo pia unahusika na kuweka utaratibu mzuri wa kukusanya taarifa na takwimu ya masuala ya elimu.

Alisema kuwa Mradi wa matumizi ya teknolojia ya kisasa katika elimu utahusisha shule 248 za msingi, kati ya hizo shule 45 zitapatiwa vifaa zaidi kwa mujibu wa sifa zilizowekwa ambapo majaribio ya mradi yameanza katika shule ya Kisiwandui na Daraji na Kituo cha Walimu Michakaeni.

Alisema kuwa vituo vyote 10 vya walimu vitapatiwa vifaa vya kisasa ili viweze kutoa mafunzo kwa walimu kwa ufanisi zaidi.